WATAFITI WAKUTANA KUJADILI MATOKEO YA TAFITI MRADI WA REGROW

Watafiti kutoka Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili, Vyuo Vikuu na wadau mbalimbali wamekutana Jijini Arusha, kujadili matokeo ya tafiti zilizofanyika katika Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dkt. Ernest Mjingo amesema jukumu kuu la TAWIRI ni kufanya, kusimamia na kuratibu tafiti za wanyamapori nchini ambapo kupitia mradi wa REGROW ina vipengele vinne (4) vya tafiti ambazo zimefanyika hivyo kikao hicho kinatoa fursa kwa watafiti kujadili matokeo ya tafiti hizo kabla ya kutumiwa rasmi.

Mratibu wa REGROW- TAWIRI Dkt. John Bukombe amesema kikao hicho ni cha siku mbili ambacho wadau watapitia matokeo ya vipengele vinne vya tafiti katika mradi wa REGROW ambavyo ni, tafiti za wanyamapori waliopo kwenye hifadhi za kusini mwa Tanzania na mtawanyiko wao, tafiti za mazingira mimea/uoto na maeneo wanyama wanapopatikana, tafiti za migongano baina ya binadamu wanyamapori na ustawi wa hali ya maisha ya jamii na tafiti za magonjwa ya wanyama hususan twiga.

Naye, Daniel Pancras ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ufugaji Nyuki kutoka Wizara ya Maliasili na utalii, amesema Matokeo ya tafiti yanasaidia kutunga sera bora ambazo zitasaidia kukuza utalii nchini na kuimarisha uhifadhi ikiwa ni kushauri njia rafiki za kutatua migongano kati ya binadamu na wanyamapori “tafiti zina umuhimu mkubwa, hatuwezi kuhifadhi bila kuwa na taarifa sahihi za kisayansi”

Profesa Flora Magige, Mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema, ipo haja ya kuwatumia wanyama wadogo na wakati kama vivutio vya utalii tofauti na sasa ambapo wanyama wakubwaa ndio wanatumika kwa wingi.

Kikao hicho kinaendelea katika Makao Makuu ya TAWIRI.

Visitors

031675
Users Today : 6
Users Last 7 days : 398
Users This Month : 1191
Total Users : 31675

Office Location

Contact Us