SERIKALI YABORESHA KIFUTA JASHO KWA WAATHIRIWA WA WANYAMAPORI  WAKALI NA WAHARIBIFU

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesikia kilio cha muda mrefu cha Wananchi wanaodhuriwa na wanyamapori wakali na waharibifu akiwemo tembo kwa kuboresha viwango vya kifuta jasho na kifuta machozi kutoka shilingi milioni moja hadi milioni mbili kwa mwananchi atakayepoteza maisha, shilingi laki tano hadi milioni moja kwa ulemavu wa kudumu na kutoka shilingi laki mbili hadi laki tatu kwa majeraha ya muda mfupi.

Akizungumza wakati wa Semina ya kuwajengea uelewa wa pamoja Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu namna Wizara inavyoshughulikia changamoto mbalimbali zinazosababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki amesema, Serikali imepokea kilio cha wananchi kwa kufanya maboresho ya Kanuni za Kifuta Jasho na Kifuta Machozi za mwaka 2011 kwa upande wa binadamu na mazao.

“Kifuta jasho kimeboreshwa ambapo kwa sasa Mwananchi atalipwa kifuta jasho cha shilingi laki moja na nusu tofauti na shilingi 37,000 za awali kwa heka kwa kuzingatia umbali wa shamba kutoka hifadhini” amefafanua Waziri Kairuki.

Aidha, Mhe. Kairuki ametoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuwahamasisha watendaji wa Halmashauri kuwasilisha wizarani kwa wakati taarifa za matukio ya vifo, majeruhi au uharibifu wa mashamba unaofanywa na wanyamapori walioainishwa kisheria kulipiwa fidia ili mchakato wa malipo kufanyika kwa wakati na kuondoa adha ya ucheleweshaji wa malipo kwa wananchi walioathirika.

Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula, akijibu baadhi ya hoja za Wabunge amesema mbali na madhara yanayosababishwa na tembo lakini pia mamba ni miongoni mwa wanyamapori wanaosababisha vifo na ulemavu kwa baadhi ya wananchi hivyo Wizara ipo katika mchakato wa kutambua maeneo ambayo matukio ya binadamu kushambuliwa na mamba yanajitokeza mara kwa mara hususan wakati wa kuchota maji tofauti na matukio yanayotokea wakati wa uvuvi ili kuanzisha matumizi ya vizimba kupunguza matukio hayo.

Mhe. Kitandula amesema hatua mbalimbali zimeendelea kuchukuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kutengeneza vifaa vya kufukuza tembo ikiwemo Mabomu baridi,
matumizi ya fensi ya mizinga ya nyuki sambamba na utoaji wa elimu ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kupunguza madhara kwa wananchi.

” Wizara inaomba kutengwa kwa bajeti ya kutosha ili vifaa hivi vitengenezwe kwa wingi na kuwafikia wananchi wengi zaidi nchini” ameeleza Mhe. Kitandula.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava amesema Wabunge wanatambua jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii za kutatua changamoto ya madhara yanayosababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo ameelekeza jitihada zaidi na tafiti kufanyika ili kupata suluhu ya kudumu.

Wakichangia kwa nyakati tofauti wakati wa Semina hiyo iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, baadhi ya Wabunge wameomba na kuhimiza Maafisa Wanyamapori kuwepo katika maeneo ya wananchi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ofisi ndogo za Maafisa hao. Vilevile, Maafisa hao wawe wenye vifaa na ujuzi wa kuwafukuza wanyamapori hususan tembo pindi wanapovamia makazi na mashamba ya wananchi hasa katika maeneo yanayozunguka Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba na Tengefu.

Visitors

031675
Users Today : 6
Users Last 7 days : 398
Users This Month : 1191
Total Users : 31675

Office Location

Contact Us