Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ubunifu wa kuvumbua bomu baridi lililoboreshwa kwa ajili ya kupambana wanyama hatari kama Tembo kwa kushirikiana na Shirika la Mzinga.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava wakati wa hafla maalum ya wizara ya Maliasili kupokea mabomu baridi 4000 yaliyo tengenezwa na Shirika la Mzinga ikiwa ni matunda ya tafiti zilizofanya kwa ushirikiano na TAWIRI.
“Nitoe pongezi za dhati kwa Wizara yetu ya Maliasili na Utalii na Shirika la mzinga kwa kuja na suluhisho hili. Natoa wito kwa Halmashauri zenye zinazopata usumbufu wa Tembo kununua na kutumia mabomu haya ili kutatua hilo” Amesisitiza Mhe. Mnzava
Ameitaka Wizara kuendelea kutoa mafunzo kwa askari wa vijiji na vijana kwa kuwa Serikali peke yake haitaweza “Hii ni kazi ya sisi sote, Serikali peke yake haitaweza ni lazima kuendelea kuwashirikisha wananchi kwa kuwapa elimu” ameongeza
Pia ameiomba Wizara kuendelea kufanya tafiti ili kubuni mbinu nzuri zaidi za kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuzingatia kuwa Tembo wamekuwa wakizoea mbinu na kuendelea kuleta usumbufu.
Mwakilishi wa wabunge kutoka kwenye majimbo yenye changamoto za Tembo walioshiriki hafla hiyo, Mhe. Salma Kikwete amempongeza Mhe. Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan na Wizara kwa kuendelea kutatua changamoto hii
“Leo kila Mbunge amefurahi kwa kuwa hili ni jambo kubwa ambalo litaleta suluhisho na sasa tunakwenda kurudisha Salam kwa wananchi wetu kazi hii nzuri iliyofanywa na wananchi” amesisitiza huku akitaka elimu iendelee kutolewa
Kwa upande wake, waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angelah Kairuki amesema wizara yake itaendelea kutekeleza kikamilifu maelekezo ya viongozi wakuu na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii.
Aidha, amesema uvumbuzi wa bomu hili baridi ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais aliyoitaka wizara kuja na ufumbuzi wa changamoto hiyo.
Ameeleza kuwa wizara yake itaendelea kuja na bunifu mbalimbali kwa kuwa hakuna njia moja pekee ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Ametumia jukwaa hilo pia kutoa pole kwa wananchi wote ambao wameathirika kwa namna moja au nyingine.
Hafla hiyo pia iliwashirikisha wabunge, Naibu Katibu Mkuu C.P Benedict Wakulyamba, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Ulinzi na menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii.