Tarehe 22 Septemba ya kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa huadhimisha Siku ya Faru Duniani (World Rhino Day) ikiwa ni mwendelezo wa lengo la kuanzishwa kwa maadhimisho hayo mwaka 2011 nchini Afrika Kusini, la kutoa elimu na kukuza uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi faru duniani.
Mtafiti wa Faru kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dkt.Victor Kakengi amesema, tafiti zimekuwa dira katika kutoa ushauri wa kisayansi wa kuhifadhi faru ikiwa ni pamoja na kubaini vinasaba (DNA) ili kuongeza uzalishaji wa faru, kutathmini maeneo yao ya asili ili kuhakikisha faru wanarejea na kustawi, kufuatilia magonjwa yanayoathiri faru na ustawi, kutumia teknolojia kufuatilia mienendo ya faru ili kubaini maeneo walipo pamoja na kuongeza ulinzi na usalama wao.
Pia, Dkt. Kakengi ameeleza tafiti za kibaiolojia zimesaidia kujua kwa kina sifa za faru za kimaumbile kama vile tabia za uzazi wa faru, muda wa kuishi, na hali ya afya ambapo taarifa hizi zinasaidia katika mipango ya kuhamasisha uzalishaji wa faru katika mazingira salama.
Akielezea historia ya idadi ya faru, Dkt. Kakengi amesema tafiti na jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika kuhakikisha idadi ya faru inaimarika ambapo miaka ya 1960 na mapema 1970 Tanzania ilikuwa ikiongoza Barani Afrika kwa kuwa na faru wapatao elfu kumi (10,000) na miaka ya 1980 na 1990 idadi ya faru ilipungua kufikia faru wasiozidi 20 katika mfumo wa ikolojia wa Serengeti.
Aidha, Serekali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi katika kuhakikisha idadi ya faru inaimarika ilianza mpango mahsusi wa ulinzi na usalama wa faru kupitia Mkakati wa Faru nchini wa mwaka 2019 hadi 2023 uliolenga kuwa na ongezeko la faru kwa asilimia 5% kwa mwaka na kufikia faru 205 mwishoni mwa mwaka 2023. Matokeo ya Juhudi hizo ni pamoja kuvuka lengo la ongezeko la asilimia 5% ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 22.09.2024 na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt.Pindi Chana, idadi ya faru imezidi kuimarika ambapo kwa mwaka huu 2024 imefikia Faru 263.
Ikumbukwe Tanzania ina aina ya faru weusi ambayo ni kati ya aina tano za faru Duniani
TAWIRI kazini.
TUMERITHISHWA & TUWARITHISHE