TEKNOLOJIA YA VIZIMBA VYA MAMBA YAREJESHA HALI YA MAISHA  YA KAWAIDA  SENGEREMA

Hali ya usalama wa maisha ya kila siku kwa wananchi waishio pembezoni mwa ziwa Viktoria  wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza yarejea baada ya Serikali  kupitia  Wizara  ya  Maliasili  na  Utalii kujenga vizimba vya kudhibiti  mamba.

Akizungumza na vyombo vya habari, Mtafiti wa Mamba kutoka  Taasisi  ya Utafiti  wa  Wanyamapori  Tanzania  (TAWIRI) Dkt.Iddi Lipende  ambaye pia ni Daktari  wa Wanyamapori  amesema, Wizara ya Maliasili  na  Utalii imeendelea kutatua migongano  kati  ya  binadamu  na Mamba kwa kutenga bajeti ya kujenga vizimba vya mfano,  ambapo mpaka sasa Wizara imewezesha ujenzi wa jumla ya vizimba sita (06) nchini na kati ya vizimba hivyo vinne (04) vimejengwa Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema.

Dkt.  Lipende amesema,  matumizi mazuri ya vizimba  vya kuzuia athari za mamba yameonyesha  ufanisi mkubwa katika kuzuia na kupunguza athari za mashambulizi ya mamba kwa wananchi ambapo tafiti zilionyesha athari zilikuwa  zikiwapata wanaotumia maji ya ziwa au mito kwa matumizi ya nyumbani kama kuchota maji, kuosha vyombo, kufua na kuoga.

” Kundi la wananchi lililokuwa likiathirika zaidi  na Mamba ni wanawake na watoto” amesema” Dkt. Lipende

Vilevile,  Dkt.Lipende amebainisha kila kizimba kimoja kina ukubwa wa upana wa mita 30 na urefu wa 35 ambapo mita 20 za uzio zipo ndani ya maji na Mita 15 zipo nchi kavu, hivyo kutoa nafasi kwa jamii  kutumia eneo hilo  kwa uhuru na usalama kwani uzio hutenganisha watu na mamba

“Pamoja na ujenzi wa vizimba hivi, jamii haina budi kufanya uangalizi  wa  karibu  kwa watoto “amehimiza  Dkt.Lipende

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Asenyi Ngaga ametoa wito  kwa wanachi kutumia vizimba hivyo kwani  licha ya Serikali  kuvijenga bado kuna  changamoto ya baadhi ya wananchi kuendelea na mazoea ya kuendelea kuoga nje ya maeneo ya vizimba, tabia ambayo *huatarisha* usalama wa maisha yao

“Hatupendi kuona watu wanapotea ndio maana tunawakumbusha wananchi wetu kuendelea kuchukua tahadhari kwa kutumia vizimba hivi” amehimiza Mhe. Ngaga

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wananchi wa Kijiji cha Nyakaliro, Halmashauri ya Buchosa wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa Vizimba hivyo ambapo wamekiri kurejesha amani na furaha kwani  vinawasaidia kuwahakikishia usalama  na kuendelea na shughuli zao za kijamii kama kawaida.

“Mwanzoni tulikuwa na shida kubwa sana ya mamba, watu walikuwa wanakamatwa watoto  wanakufa kwa ajili ya mamba lakini kutokana na hiki kizimba amani imerejea, tunaishukuru Wizara  ya  Maliasili  na taasisi zake  za TAWIRI  na TAWA kwa kutujengea hiki kizimba amesema”  Elizabeth  John Mkazi wa Kijiji cha Nyakaliro.

Nae, Beatus Maganja kutoka TAWA, amesema kuanzia Julai 2023 hadi Mei 2024 TAWA ilifanya jumla ya mikutano 84 ya kutoa elimu ya uhifadhi na mbinu mbalimbali za kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko katika vijiji 44 na shule 40 ambapo  jumla ya watu 53,639 walifikiwa na elimu hiyo

Ikumbukwe, ujenzi huu wa vizimba  vya jamii vya kuzuia mamba umefadhiliwa na Wizara  ya  Maliasili  na  Utalii  kupitia  Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori (TWPF) na TAWA amba vizimba hivyo sita (06) vya mfano vimejengwa katika Vijiji vya  Kanyala, Izindabo, Nyakaliro na Nyachitare wilaya ya Sengerema Mkoani  Mwanza na vizimba  vinne  vimejengwa Rukwa na Iboma wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe.

Visitors

028303
Users Today : 5
Users Last 7 days : 689
Users This Month : 2229
Total Users : 28303

Office Location

Contact Us