Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) kwa kuthamini umuhimu wa wadudu katika sekta ya uhifadhi na kuanzisha maabara maalumu ya kuwahifadhi wadudu wote wanaopatikana hapa nchini na nchi nyingine.
Waziri Kairuki ametoa pongezi hizo katika maonyesho ya Karibu Kili Fair 2024 ambayo yamehitimishwa leo 9 Juni, 2024 jijini Arusha ambapo pia ameelekeza taasisi hiyo kuona fursa za utalii katika swala zima la wadudu .
Aidha, ikiwa tafiti chache za wadudu zimefanyika katika nchi nyingi zinazoendelea huku kipaumbele kikitolewa kwa wanyamapori wakubwa , TAWIRI inajivunia
kuwa na Maabara hii ya wadudu ambayo ni kituo muhimu na sahihi kwa ajili ya kuhifadhi makundi mbalimbali ya wadudu yanayofanyiwa utafiti .
Akizungumza na Mwanahabari wetu, Mtafiti wa Wadudu kutoka TAWIRI Neema Kilimba amesema kupitia maabara ya Wadudu, TAWIRI kwa kushirikiana na wadau wengine inakamilisha Kanzidata ya makundi mbalimbali ya wadudu wanaopatikana Tanzania na nchi nyingine.
Vilevile kupitia maabara hii, TAWIRI inaandaa orodha ya makundi mbalimbali ya wadudu na mtawanyiko wao nchini (atlas of insects) wakiwemo nyuki, mbawakawa wanaoviringisha vinyesi (dung beetles), wadudu wa maji baridi (aquatic insects of fresh water) na mbawakawa wanaoishi ardhini (carabidae – beetles)
Mtafiti Kilimba amebainisha, uwepo wa kanzidata ya makundi mbalimbali ya wadudu utasaidia kutambua aina mbalimbali za wadudu tulizonazo pamoja na makazi na mtawanyiko wao hivyo kuchochea uhifadhi wa bioanuwai hii muhimu, kutoa elimu na msingi wa takwimu kwa watafiti na wanafunzi mbalimbali.
” uwepo wa maabara ya wadudu umeamsha ari ya watafiti na wanafunzi kusoma na kufanya tafiti za wadudu ambao wanamchango mkubwa katika maisha ya binadamu, wanyama na mimea” amesema Mtafiti Kilimba
Ameongeza Wadudu wanachangia uchavushaji wa mimea kwa zaidi ya asilimia 80%, uozeshaji na umeng’enyaji wa taka hususani vinyesi na usafishaji wa mazingira(decomposition), uoteshaji wa mbegu mbalimbali, uongezaji mbolea kwenye udongo ( soil fertilization ), kuwezesha makazi ya wanyama wengine. Pia Wadudu ni chakula kwa wanyama wengine na sehemu muhimu kwenye mzunguko wa chakula (food chain)
Vilevile wadudu wanatumika kama viashiria vya afya ya mifumo ya kiikolojia. Wadudu wanachangia kwa asilimia kubwa kuongeza kipato kwa jamii kwa kuuza wadudu wenyewe kama chakula au bidhaa zitokanazo na wadudu.
TAWIRI inawakaribisha wadau mbalimbali kujifunza kuhusu wadudu na ufugaji bora wa nyuki. Pia tunatoa elimu ya kisayansi (Scientific talks) kuhusu wadudu na wanyamapori wengine kwa wadau wa utalii, wanafunzi na watafiti sambamba na kutoa ushauri (consultancy) ya uwekezaji kwenye sekta ya utalii.